7 Julai 2025 - 23:09
Source: Parstoday
Jenerali Shekarchi: Iran itatoa jibu la kuponda zaidi iwapo Israel itaishambulia tena

Kamanda mwandamizi wa Jeshi la Iran ameonya kuwa, Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu viko tayari kufanya mashambulizi yenye nguvu na ya maangamizi zaidi dhidi ya vitendo vyovyote vya kichokozi vitakavyofanywa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya taifa hili.

Brigedia Jenerali Abolfazl Shekarchi, Msemaji wa Vikosi vya Wanajeshi wa Iran, aliyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Defapress kuhusu ukiukaji wa usitishaji vita unaoweza kufanywa na Israel na hatua za kulipiza kisasi za Iran.

"Majibu yetu kwa mashambulizi yoyote tarajiwa ya utawala unaoikalia kwa mabavu al-Quds yatakuwa na sifa ya kuongezeka kwa nguvu, ukali, ufanisi, na kiwango cha matokeo ambacho kitaibua majuto makubwa," amesema.

Akizungumzia matamshi ya wataalamu wa kimataifa kuhusu ushindi wa Iran dhidi ya utawala wa Israel, Brigedia Jenerali Shekarchi amesema, "Tulishinda vita vya siku 12 na kutoa pigo kubwa kwa utawala wa Kizayuni."

Brigedia Jenerali Abolfazl Shekarchi ameashiria kisasi kikali cha mfululizo cha Iran dhidi ya utawala huo pandikizi na kueleza kuwa, "Tuliulazimisha utawala huu wa kihalifu kusitisha uchokozi wake kupitia hujuma zetu."

Kamanda huyo wa ngazi ya juu wa Jeshi la Iran amesisitiza juu ya utayarifu wa hali ya juu ndani ya vikosi vya jeshi la Iran, na kutoa onyo kali kwa kusema: "Iwapo utawala wa Kizayuni utaanzisha hatua yoyote zaidi (dhidi ya Iran), watakabiliwa na jibu kali."

Siku ya Ijumaa, Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Brigedia Jenerali Ali Mohammad Naeini alisema Iran haitazingatia tena mstari wowote mwekundu iwapo utawala wa Israel utafanya kitendo kingine cha uchokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Your Comment

You are replying to: .
captcha